1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Rice Barani Asia

16 Machi 2005

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condolezza Rice asifu masikizano kati ya India na Pakistan

Condolezza Rice
Condolezza RicePicha: dpa

Katika ziara yake ya mataifa sita ya bara Asia bibi Rice ameusifu ushirikiano na uelewano mzuri baina ya mataifa ya India na Pakistan ambayo katika kipindi cha miaka kadhaa yamekuwa yakizozana.

Waziri wa mambo ya nje nchini India Natwar Sigh amesema katika mkutano wa pamoja na waandishi habari, kuwa ni jambo lililo wazi kudumisha amani kati ya nchi yake na Pakistani lakini akaongeza kusema kuwa ni muhimu kwa Pakistan kujitolea kikamilifu kumaliza vitendo vya kigaidi katika mipaka yake dhidi ya India.

Serikali ya India inaishutumu Pakistan kwa kufadhili makundi ya waasi katika eneo la Kashmir,ambalo limegawanyika kati ya nchi mbili.

Lakini Islamabad imekanusha madai hayo na kudai kuwa kamwe haijawahi kuunga mkono harakati za kujikomboa kwa wakashmir.

Katika mazungumzo yao Rice na Sigh pia waligusia suala juu ya maendeleo katika Nepal, ambapo mfalme wa nchi hiyo Gyanedra, mwezi uliopita alilifuta kazi baraza lake la mawaziri na kuchukua mamlaka yote mwenyewe. Na hivyo Rice amesema ipo haja kwa Nepal kurejea kwenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa.

Bibi rice alipoulizwa kuhusu uwezekano wa marekani kuiuzia India ndege za kivita aina ya F 16, alijibu kwamba suala hilo limechomoza lakini makubaliano yaliyoafikiwa kuhusiana na hilo hayawezi kutolewa kwa sasa na kwamba suala hilo litazungumziwa zaidi katika mkutano wa Islmabad baadae wiki ijayo.

Upande wake waziri wa mambo ya nje wa India bwana Singh, amedokeza kwamba kuuzwa kwa ndege hizo kwa Islamabad huenda kukazua matatizo lakini akaongeza kusema kuwa hakujakuwepo na tofauti kubwa baina ya mawazo yake na bibi Rice.

Mvutano kati ya Pakistani na India umetulia kwa kiasi, tangu kufanyika mazungumzo kati ya nchi hizo mbili mwaka uliopita uliodhamiria kumaliza uhasama wa zaidi ya miongo minne.

Lakini New Delhi imeipinga vikali Marekani kuiuzia Pakistan silaha ikiwa ni pamoja na ndege za kivita aina ya F16,ikisema kuwa silaha hizo zinadhamiriwa kutumika dhidi ya India.

Hata hivyo Marekani pia inadhamiria kuiuzia India ndege hizo za kivita.

Washington iliiuzia Pakistan ndege hizo za aina ya f 16 katika mwaka 1980 ambapo Islamabad iliisaidia kuondosha usovieti nchini Afghanistan.

Lakini shehena hiyo ilizuiwa kuanzia mwaka 1990 baada ya kupitishwa sheria ya Marekani ya kuzuia kupelekwa silaha za kijeshi nchini Pakistan ambapo ilitiliwa shaka kuhusika kuwa na zana za kinuklea.

Wakati huo huo Pakistan inataka kujiunga na kundi la kimataifa la kupambana na kuenea kwa silaha za nuklea na kwa mujibu wa maafisa nchini humo huenda ikazusha suala hilo wakati wa ziara ya bibi Rice.

Serikali ya Pakistan wiki iliyopita ilikiri mwanasayansi wake wa hadhi ya juu anayehusika na mambo ya nuklear Abdul Kadeer Khan,alitoa ufundi wa kutengeneza silaha za nuklea kwa Iran lakini akasisitiza kwamba serikali haikuhusika katu katika sakata hilo.

Khan hivi sasa yupo chini ya kifungo cha ndani tangu mwaka 2003 baada ya kukiri kutoa ujuzi huo kwa Korea Kaskazini, Libya na Iran.