Ziara ya Ujumbe wa baraza la Usalama la UN
7 Oktoba 2013Kikosi kipya maalumu cha jeshi la Umoja wa Mataifa huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kimefanikisha ushindi wa kijeshi dhidi ya waasi wa M23 na kulazimisha waasi hao waunge mkono mazungumzo ya amani. Kikosi hicho kwa hivi sasa kinabadili mwelekeo na kuyageukia makundi mengine mawili hatari yenye silaha nchini humo.
Katika ziara ya wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini Goma, hapo jana(06.10.2013), Mkuu wa Ujumbe wa Monusco alisema kwamba wakati kundi la waasi la M23 likigonga vichwa vya habari duniani ndivyo pia kinavyoonekana kuongezeka kitisho kinachosababishwa na waasi wa kundi la FDLR kutoka nchi jirani ya Rwanda pamoja na kundi la itikadi kali la ADF.Mkuu wa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa Monusco,Ray Torres anasema ikiwa kikosi hicho hakitofanikiwa kwa njia moja au nyingine kusawazisha hali ya mambo na kuwapokonya silaha pamoja na kuyavunja makundi hayo hakutakuwepo matumaini makubwa ya kurejeshwa amani na utulivu katika eneo hilo.
Makundi ya waasi
Kwa mujibu wa Torres makundi 39 mengine yenye sialaha katika mashariki ya Kongo yanahalalisha kuwepo kwao kwa kisingizio cha kukabiliana na M23 na FDLR.Mamilioni ya watu wamepoteza maisha yao kutokana na ghasia vurugu,magonjwa na njaa tangu miaka ya 1990 wakati makundi ya waasi yakipambana kuyadhibiti maeneo yenye utajiri wa dhahabu almasi shaba,madini ya Cobalt na Urani mashariki ya Kongo.
Itakumbukwa kwamba mapema mwaka huu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliunda kile ilichokiita brigedia maalum ndani ya Monusco iliyopewa kibali cha kuingilia kati kijeshi pale inapohitajika kukabiliana na waasi,ikiwa ni hatua mpya kabisa kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa katika kikosi chake cha kulinda amani ambacho kwa miaka kadhaa kimekuwa kikikosolewa katika eneo hilo kwa kutochukuwa hatua yoyote pamoja na kushindwa kuwalinda raia.Wanajeshi wa Malawi walianza kuingia wiki iliyopita kujiunga na wanajeshi kutoka Afrika Kusini na Tanzania katika kikosi hicho maalum cha wanajeshi 3000.
Jukumu la Monusco
Kikosi cha kuweka amani cha Umoja wa Mataifa Monusco kina jumla ya wanajeshi 20,000 waliotawanywa kote katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Mkuu wa kikosi hicho Ray Torres ambaye aliungoza ujumbe wa maafisa 15 wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika ziara yao hapo jana aliwepeleka pia katika eneo la mlima linalofahamika pia kama Kibati huko kaskazini ya mji wa Goma ambako ndiko zilikoanzia operesheni za kikosi cha kongo kikisaidiwa kwa mara ya kwanza na brigedia maalum ya Monusco ,operesheni iliyobadilisha hali nzima ya mambo ikiwa ni pamoja na kuwatimua M23 mwezi Agosti na kuwalazimu waasi hao kukubali mazungumzo.
Hata hivyo licha ya mafanikio hayo wajumbe wa baraza la usalama la Umoja huo wa Mataifa wamepinga kile walichokiita matarajio ya kupita kiasi yaliyowekewa kikosi hicho,pale walipoingia kwenye mazungumzo na maafisa wa Kongo huko Kinshasa siku ya Jumamosi pamoja na viongozi wa mashirika ya kiraia mjini Goma hapo jana.Raia wa mashariki ya kongo wanaamini kwamba ni kikosi cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kuyamaliza makundi yote yenye silaha katika eneo hilo.
Wakati huohuo Ujumbe huo wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa umesema Marekani na Uingereza zinaitia msukumo serikali ya Kongo kuwashtakiwa wanajeshi waliohusika kuwabaka huko Minova kiasi wanawake 130 na wasichana.Suala hilo liliibuka katika mazungumzo kati ya wajumbe hao na mawaziri wa Kongo wanaohusika na ulinzi,mambo ya ndani na sheria siku ya Jumamosi.
Mwandishi:Saumu Yusuf
Mhariri: Mohammed AbdulRahman