Jiabao atembelea Umoja wa Ulaya
30 Januari 2009China na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuitisha mkutano wa viongozi wa pande hizo haraka, baada ya mkutano uliopangwa kufanyika hapo awali kuahirishwa, kutokana na kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama kufanya ziara katika nchi fulani za Umoja wa Ulaya.
Rais wa tume ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barosso, amesema hayo leo mjini Brussels baada ya mazungmzo yake na waziri mkuu wa China, Wen Jiabao, anaefanya ziara barani Ulaya.
Bwana Barosso amewaambia waandishi habari kwamba mkutano baina ya viongozi wa China na wa Umoja wa Ulaya utafanyika haraka iwezekenavyo.
Bwana Barosso amesema kuwa Ulaya ina dhamira kubwa katika kushirikiana na China.
Ziara ya waziri mkuu wa China, Wen Jiabao, barani Ulaya ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa ngazi za juu wa China tokea kuahirishwa mkutano uliopangwa kufanyika hapo awali kutokana na suala la Dalai Lama, kiongozi wa kidini wa Tibet aliekutana na baadhi ya viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya.Hatua hiyo iliikasirisha China na iliamua kuvunja mkutano huo uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka jana.
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa alikuwa miongoni mwa viongozi wa Ulaya waliokutana na Dalai Lama.
Kwa mujibu wa China, Dalai Lama anaendesha harakati zenye lengo la kulitenga jimbo la Tibet na China.
Akizungumzia ziara yake barani Ulaya, waziri mkuu wa China, Wen Jiabao, amesema kuwa ziara hiyo imeinua hali ya kuaminiana na uelewano baina ya nchi yake na Umoja wa Ulaya.