1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zilzala ya kisiasa kufuatia uchaguzi wa bunge nchini Austria

Hamidou, Oumilkher29 Septemba 2008

Mizozano ya serikali ya zamani ya muungano yaitumbukiza Austria mikononi mwa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia

Kiongozi wa chama cha Social Democratic SPÖ Werner FaymannPicha: picture-alliance/dpa




Zilzala ya kisiasa imepiga nchini Austria kufuatia ushindi mkubwa wa vyama vya siasa kali ya mrengo wa kulia dhidi ya wasocial Democratic na wahafidhina katika uchaguzi wa bunge uliotishwa kabla ya wakati hapo jana.



"Wapiga kura wamelalamika dhidi ya maendeleo finyu ya washirika wa muungano mkuu wa zamani-wa mrengo wa kushoto na kulia,uliovunjika July iliyopita baada ya miezi 18 ya kupooza shughuli za serikali"-anafafanua hali hiyo mtaalam wa masuala ya kisiasa Peter Hofer."Waaustria wamekasirika kwanamna ambayo wamekwenda kupiga kura wakiwa na hasira kweli kweli" amesema hayo mhariri wa gazeti la Standard.


Risala ya wapiga kura wa Austria ni bayana:wasocial Democratic -SPÖ wameteremka kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya chama chao chini ya kiunzi cha asili mia 30-wamejipatia asili mia 29.7 na wahafidhina wa ÖVP wakipata pigo kubwa na kuteleza hadi kiunzi cha asili mia 25.6.


Badala yake mrengo wa kulia,zikichanganywa kura za makundi yote mawili,chama cha FPÖ cha Heinz-Christian Strache na chama cha BZÖ cha Jörg Haider,kwa pamoja wamejikingia asili mia 29-takriban sawa na wasocial Democratic wanaoendelea kua chama kikuu cha kisiasa nchini Austria.


Kwa mujibu wa gazeti la Die Presse "zilzala hii inamaanisha kuchoshwa waustria na mivutano isiyokwisha ya vyama vikuu,vinavyoshindwa kutia njiani mageuzi yanayosubiriwa ya kodi ya mapato- mojawapo ya ahadi muhimu walizotoa katika kampeni za uchaguzi mnamo mwaka 2006.


Wakisaidiwa na ughali wa maisha na pia mzozo wa fedha wa Marekani unaoanza kuingia pia katika nchi za Ulaya ya magharibi,wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia walilenga zaidi mada za kijamii katika kampeni zao za uchaguzi.Mada zao zinaonyesha kuwavutia sana vijana na wafanyakazi wa kawaida.


Kiongozi mpya wa chama cha Social Democratic SPÖ-Werner Faymann anasema:


"Bado kuna idadi kubwa ya wapiga kura tunaobidi kuwazindua.Na hiyo ndio sehemu ya matokeo ya uchaguzi ambayo nnabidi kuishughulikia"


Chama cha Social Democratic cha SPÖ na kiongozi wake Werner Faymann wana kazi ngumu ya kujipatia mshirika kuunda serikali ya muungano.


Tangu jana usiku Werner Faymann alisema wanapendelea serikali itakayodhamini utulivu,akiondowa uwezekano wa kushirikiana na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia.


Kwa maoni yake serikali mpya ya muungano wa vyama vikuu inawezekana tuu ikiwa viongozi wepya watachaguliwa kutoka chama cha kihafidhina.


Wakati huo huo halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya imeelezea matumaini yake kuiona Austria ikiendekea kutoa mchango wa maana katika Umoja wa Ulaya.






Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW