1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe bila ya Mugabe madarakani, hali ikoje?

14 Novemba 2018

Mwaka mmoja uliopita nchini Zimbabwe kilitokea kitu ambacho hakikutegemewa. Robert Mugabe aliondolewa madarakani. Magari ya kijeshi yalitawala katika mitaa ya mji mkuu Harare Novemba 14 mwaka 2017 .

Zimbabwe's former president Robert Mugabe looks on during a press conference at his private residence nicknamed "Blue Roof" in Harare
Picha: Reuters/S. Sibeko

Mnamo tarehe 14 Novemba jeshi likamuweka katika kifungo cha nyumbani kiongozi huyo mkongwe wa Zimbabwe, katika kujibu hatua ya Mugabe kumfukuza kazi makamu wake wa rais wakati huo Emmerson Mnangagwa. Mwaka mmoja tangu alipoondolewa madarakani Robert Mugabe, Je kuna mabadiliko yoyote?

Mamia kwa maelfu ya Wazimbabwe walicheza na kushangilia kwa furaha katika mitaa ya miji mbali mbali kusherehekea kumalizika kwa enzi ya utawala wa ukandamizaji wa Mugabe ambao ulichangia katika kuuharibu kabisa uchumi wa taifa hilo uliowahi wakati mmoja kuwa thabiti. Mugabe ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 92 alijiuzulu mara moja na kuumaliza utawala wake uliodumu miaka 37.

Mwaka mmoja baade matatizo ya kiuchumi ya Zimbabwe yameongezeka huku uhuru wa msingi ukiendelea kubanwa hali ambayo inawafanya baadhi ya wazimbabwe kujiuliza ni kitu gani hasa kilichobadilika? na je kuna ubora wowote? Ile furaha iliyokuweko Mugabe alipoangushwa madarakani imetoweka.Mnangagwa aliwaahidi Wazimbabwe ukurasa mpya lakini wengi nchini humo wanaonekana kubughudhika hasa bado inapoonekana misururu mirefu kwenye mabenki watu wakienda kutowa miburungutu ya pesa pamoja na upungufu mkubwa wa bidhaa za msingi ambao umechangia hata kuwepo hali ya mgao wa mafuta ya kupikia ,maji ya kunywa ya chupa pamoja na bia.

Wananchi wa Zimbabwe wakiimba na kushangilia kumshinikiza Mugabe kuachia madaraka, 2017Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Mkaazi mmoja wa Harare kwa jina Andrea Magoronye anasema walidanganywa,na kuandamana pasipo sababu ya msingi.Marogoye ni mkaazi wa mji mkuu Harare anazungumza hayo akiwa amesimama kwenye msururu mrefu wa kusubiri kununua mafuta ya kupikia kwenye duka la Supermarket.

Mnangagwa alianza vizuri uongozi wake lakini ushindi wake uliozusha utata katika uchaguzi mnamo mwezi Julai mwaka huu ulifuatiwa na hatua za jeshi kufyetua risasi na kuua watu sita,raia wasiokuwa na hatia.Mripuko wa Cholera ulifuatia na hali ngumu ya kiuchumi  ndo kwanza imezidisha mashaka juu ya uongozi wa mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 76 katika mwaka wake wa kwanza madarakani.

Mnangagwa aliaahidi kuugeuza uchumi ulioporomoka wa Zimbabwe kuwa wa kiwango cha kati kufikia mwaka 2030 ,kuanzisha msingi wa mageuzi ya demokrasia,na kujisogeza tena katika ushirikiano na Marekani pamoja na nchi nyingine za Magharibi ambazo ziliiweka Zimbabwe chini ya vikwazo wakati wa Mugabe. Vikwazo hivyo bado havijaondolewa na hakuna ishara zinazoonesha uhakika wa hilo kutokea. Mnamo mwezi Septemba mfumko wa bei za bidhaa ulipanda na kufikia kiwango cha juu zaidi ambacho hakijawahi kuonekana tangu mwaka 2010 kwa mujibu wa shirika la kitaifa la takwimu Zimstat.

Rais Emmerson Mnangagwa akiwasalimu wafuasi kwenye mkutano wa kampeni Picha: Reuters/P. Bulawayo

Kuna upungufu wa dawa katika nchi nzima ambayo toka hapo mfumo wake wa afya umekwisha karibia kusambaratika muda mrefu. Maduka ya dawa ya binafsi yenye dawa yanauza dawa zao kwa dolla za kimarekani,fedha ambazo hazipatikani kirahisi nchini Zimbabwe.

Zimbabwe inaondokana taratibu na mripuko wa maradhi ya kipindupindu ugonjwa ambao rais ameutaja kama ni ugonjwa wa kizamani ambao umeshawauwa takriban watu 50 katika mji mkuu Harare. Wengi wanahofia  mgogoro wa sasa umechochewa na upungufu wa fedha za kigeni pamoja na kuongezeka kwa deni la nchi na kwa mujibu wa shirika la fedha duniani IMF hali hiyo huenda ikawa mbaya zaidi na kugeuka kuwa mgogoro wa kiuchumi ambao haujapata kuonekana kwa kipindi cha muongo mmoja nchini Zimbabwe, pale ambapo mfumko wa bei ulifikia asilimia billioni 500.

Juu ya hilo wanaomkosoa rais Mnangagwa wanasema serikali yake bado inawakandamiza watu huku ikitajwa kwamba kuna watu chungunzima waliokamatwa kwa tuhuma za kumkosoa rais,ukandamizaji ambao ni sawa na uliokuwa ukifanywa na utawala wa Mugabe.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri.Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW