Zimbabwe kupitisha sheria mpya ya ujenzi
11 Mei 2022Zimbabwe inapanga kupitisha sheria mpya kuhusu ujenzi wa nyumba. Sheria hizo zinalenga kusaidia jamii za vijijini ziweze kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yakiwemo upepo mkali na mvua kubwa zinazo sababisha mafuriko.
Kulingana na takwimu za serikali nchini Zimbabwe kuanzia 2017, zimeonyesha kuwa asilimia 80 ya nyumba katika maeneo ya vijijini zimejengwa kwa matofali ya udongo ambayo ni mbinu ya jadi , na asilimia 98 ya nyumba katika maeneo ya mijini zimejengwa kwa matofali ya saruji ambayo ni mbinu ya kisasa.
Florence Panda, ni raia nchini Zimbabwe anayeishi kwenye nyumba mpya iliyojengwa muundo wa kisasa , baada ya kupoteza nyumba yake ya awali katika kijiji cha Ndiadzo, huko Jimbo la Manicaland mashariki mwa nchi hiyo, kutokana na upepo mkali na mvua za mafuriko zilizonyesha Zimbabwe mwaka 2019, na kuharibu takriban nyumba 50,000.
''Tuliishi kwenye mahema''
Mvua kubwa iliyonyesha ilisomba nyumba ya panda aliyoijenga kwa matofali ya udongo wa kichuguu na kusababisha familia ya Panda kukosa makazi.
"Ilikuwa huzuni kupoteza makazi yetu na kila kitu kwa usiku mmoja tu,” Panda aliliambia Shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu.
"Kwa zaidi ya mwaka mmoja, tuliishi kwenye mahema, tulifurahi kupata makazi mapya kwani ilikuwa ahueni ."
Mwaka mmoja baadaye, Panda na familia yake walihamia kwenye nyumba za kisasa zilizojengwa vijijini na serikali, zenye viwango vya kuhimili mvua kubwa na upepo mkali.
Miradi ya serikali kwa wathiiriwa wa majanga
Percy Toriro, mtaalamu wa mipango miji aliyepo mjini Harare, alisema hii ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba za kisasa maeneo ya vijijini na zitakuwa na ubora kama nyumba za mijini." makazi ya mijini yamekuwa salama zaidi kutokana na udhibiti wa viwango na ubora nyumba ambapo, makazi ya vijijini hayakuwahi kudhibitiwa viwango au ubora wowote," alisema.
Mnamo mwaka 2020, serikali ya Zimbabwe ilipitisha sera na sheria mpya ya ujenzi wa nyumba na kujenga nyumba za kisasa 700, kwa watu walioathiriwa na majanga ya asili., alisema Nathan Nkomo, mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi wa Raia, kwenye shirika la Serikali la kukabiliana na maafa, ambalo lilisaidia kuunda viwango vipya vya ujenzi.
Sera mpya ya makazi, inaitaka mabaraza ya vijijini kuhakikisha majengo yote mapya ya vijijini yanajengwa kisasa, kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa, alisema David Mutasa,mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makoni Vijijini.
Hifadhi ya mazingira
Ili kuzuia uharibifu wa mazingira, sera inapiga marufuku ujenzi wa vibanda vya mbao kwenye maeneo ya vijijini na ujenzi kwenye maeneo ya bondeni ili kujikinga na majanga ya asili.Nchini Zimbabwe, adhabu ya ukataji miti bila kibali ni kati ya dola 5,000 na 50,000 za Zimbabwe ($13-$133).
Sio kila mtu amefurahia sera mpya ya makazi, na baadhi ya viongozi wa eneo hilo wamesema wamekabiliwa na shinikizo.Nyumba za jadi, unaweza kujenga kutumia udongo na mbao bila gharama yoyote,alisema Toriro, mtaalam wa mipango.
"Baadhi ya watu hawana fedha za kujenga nyumba za kisasa kutokana na viwango vinavyohitajika,” alisema. Florence Panda ambaye alitumia $500 kuongeza vyumba vitatu zaidi kwenye nyumba yake mpya iliyojengwa na katika kijiji cha Ndiadzo.