Zimbabwe magazetini
23 Juni 2008
Vuta nikuvute katika chama cha Social Democratic-SPD,mkutano wa kilele wa nchi zinazochimba na zile zinazotumia mafuta kwa wingi duniani mjini Djiddah nchini Saud Arabia na tangazo la chama cha upinzani cha Zimbabwe kususia duru ya pili ya uchaguzi wa rais, ndizo mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.
Tuanzie Zimbabwe ambako Morgen Tsvangirai anasema hatoshindana na rais Robert Mugabe katika rauni ya pili ya uchaguzi wa rais.Gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER linachambua:
"Vitisho na vifo-hoja za Tsvangirai za kutoshiriki katika duru ya pili ya uchaguzi zinaeleweka.Lakini wakati huo huo uamuzi uamuzi huo unamaanisha kukitumukiza kaburini chama hicho cha upinzani.Mugabe anapewa madaraka bure.Matokeo yake ni bayana:vitisho dhidi ya upinzani vitaongezeka,mparaganyiko wa kiuchumi utazidi,njaa itaenea na usumbufu na shida itaongezeka.Upande wa upinzani umesalim amri hata kabla ya kulifikia lengo lake.
"Zimbabwe itazidi kudidimia" anahofia kwa upande wake mhariri wa gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG,na kuendelea kuandika:
Nchi hiyo imetumbukia katika janga la njaa,na wananchi wake watazidi kutaabika.Kujitenga upande wa upinzani kunampokonya Mugabe nafasi ya kujivika kilemba cha ukoka kama mpenda demokrasia.Atazidi kupoteza chembe ya imani iliyomsalia akijitangaza mshindi wa uchaguzi.Jumuia ya kimataifa na hasa mataifa jirani ya Afrika wanabidi kumueleza kinaga ubaga Mugabe,kwamba utawala wake wanauangalia kama madaraka ya wizi.Wanabidi wajiepushe kushirikina na muimla huyo na kusimama kidete dhidi ya serikali ya mjini Harare.Hawastahiki kuendelea kuvifumbia macho visa vya dhalimu huyo."
Maoni sawa na hayo yametolewa na gazeti la HANDELSBLATT linaloitolea mwito zaidi Afrika kusini iwajibike.
Mada ya pili magazetini inahusu mkutano wa kilele wa Djiddah kati ya viongozi wa mataifa yanayochimba mafuta kwa wingi duniani na wale wa mataifa yanayotumia kwa wingi bidhaa hiyo.
Gazeti la Die Welt linaandika:
"Mkutano huo wa mafuta ulioitishwa na Saud Arabia ulizusha matumaini makubwa walimwengu wakijiuliza kama nchi hiyo inayoongoza katika kuchimba mafuta duniani,italitumia kweli jukwaa la OPEC kutangaza azma ya kuzidisha kiwango cha mafuta.Ishara kama hiyo ingekua ya nguvu kuweza kushawishi bei ya mafuta katika soko la kimataifa.Pengine hata mfumko wa bei ya mafuta ungenyweya.Lakini hakuna ishara yoyote iliyotolewa.Mfalme Abdallah na waziri wake wa mafuta Al Naimi wamethibitisha kile kinachojulikana tokea hapo kuhusu kuongezwa kiwango cha mafuta na kuzungumzia umuhimu wa kuwepo hali ya uwazi na kuahidi kubuni fuko la misaada kwaajili ya mataifa yasiyo jimudu.Hayo ni haba linasema gazeti la Die Welt.
Gazeti la RHEIN-NECKAR-ZEITUNG la mjini Heildelberg linahisi:
"Saud Arabia na Kuweit wanazidisha kiwango cha kuchimba mafuta.Habari nzuri.Lakini kama zitasaidia kubadilisha chochote katika bei inayozidi kupanda ya mafuta,hilo ni suala jengine.Enzi za mafuta ya bei hafifu zimeshapita.Ingawa machimbo mepya ya mafuta yanagunduliwa hapa na pale na kuzusha matumaini ,lakini katika maeneo ya mbali sana na kina cha chini pia kupita kiasi kwa hivyo kuyachimba ni kazi na ghali."
►◄