1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe: Mripuko wa surua yawaua watoto 80

15 Agosti 2022

Mripuko wa ugonjwa wa surua umewaua watoto 80 nchini Zimbabwe tangu mwezi Aprili. Hayo yamesemwa na wizara ya Afya ambayo imeelekeza lawama kwa mikusanyiko ya kanisa kusababisha ongezeko la mripuko huo.

Afrika Kongo Masern Impfung
Picha: Getty Images/J. Kannah

Kwenye taarifa ambayo shirika la habari la Reuters limepata nakala yake, wizara ya Afya imesema mripuko huo umeenea nchini kote huku viwango vya vifo vikiwa 6.9%.

Mnamo Alhamisi, waziri wa Afya Jasper Chimedza  alisema watoto 1, 036 walishukiwa kuambukizwa, 125 walikuwa wamethibitishwa kuugua ugonjwa huo tangu mwanzo wa mripuko, huku eneo la Manicaland mashariki mwa Zimbabwe likirekodi maambukizi mengi.

"Wizara ya Afya ingependa kufahamisha umma kwamba mripuko wa ugonjwa wa surua unaoendelea na ambao uliripotiwa mwanzo Aprili 10, sasa umeenea nchini kote kutokana na mikusanyiko ya watu makanisani,” Chimedza alisema kupitia taarifa.

Niger yaruhusu chanjo ya malaria kwa watoto

"Mikusanyiko iliyowaleta watu kutoka mikoa mbalimbali na ambao rekodi zao za chanjo hazijulikani, zilisababisha surua kuenea hadi maeneo ambayo awali hayakuwa yameathiriwa.”

Katika Manicaland, mkoa wa pili kwa wingi wa watu nchini Zimbabwe, visa 356 vimeripotiwa na vifo 45, Chimedza amesema.

Askofu Andby Makuru, kiongozi wa dhehebu la Johanne, hakutoa kauli ya moja kwa moja alipotumiwa swali.

Watoto walioripotiwa kuambukizwa zaidi ni walio na umri wa kati ya miezi sita hadi miezi 15, hususan waumini ambao watoto wao hajapata chanjo dhidi ya surua kutokana na imani za kidini, aliongeza.Picha: DW/C. R. Matonhodze

Nchini Zimbabwe,baadhi ya madhehebu huwakataza waumini wao kupokea chanjo au matibabu ya hospitali. Makanisa hayo ambayo hutoa ahadi za kuponesha maradhi na kuwakwamua watu kutoka kwenye minyororo ya umaskini, yana mamilioni ya waumini.

Kwa nini ugonjwa wa surua umeitesa sana DRC?

Huku viwango vya upokeaji chanjo vikiwa chini katika baadhi ya maeneo, pamoja na ukosefu wa rekodi za chanjo, serikali imeamua kuanzisha kampeni ya kutoa chanjo kwa umma katika maeneo ambayo mripuko uliripotiwa.

Mripuko hu owa surua unatarajiwa kudhoofisha sekta ya afya ambayo tayari imeathiriwa na ukosefu wa dawa na vilevile migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi wa afya.

Mnamo Julai ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema ongezeko la taarifa za kupotosha, pamoja na kuathiriwa kwa minyororo ya usambazaji chanjo kimataifa uliosababishwa na janga la COVID, ni miongoni mwa mambo makubwa yaliyosababisha kasi ya utoaji chanjo kwa watoto kushuka zaidi katika miongi mitatu iliyopita.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa mwezi Julai, 2022 ilisema watoto milioni 25 walikosa chanjo muhimu dhidi ya maradhi kama kifaduro na pepopunda.Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Mednick

Kulingana na data rasmi ya ripoti hiyo iliyochapishwa na Shirika la Afya Duniani pamoja na shirika la Watoto UNICEF, asilimia ya watoto waliopokea dozi tatu za chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda na kifaduro, ilishuka kwa asilimia tano kati ya mwaka 2019 na 2021 hadi 81%.

Katika mwaka 2021, takriban watoto milioni 25 walikosa chanjo dhidi ya kifaduro, hiyo ikiwa milioni mbili zaidi ya waliokosa chanjo hiyo mwaka 2020 na vilevile milioni sita zaidi ya wale waliokosa chanjo hiyo mwaka 2019, hali inayoweka maisha ya watoto katika hatari.

Taarifa ilisema wengi wa watoto ambao walikosa chanjo hizo muhimu mwaka 2021 huishi katika nchi zenye mapati ya chini na wastan. Ethiopia, India, Indonesia, Nigeria na Ufilipino zilirekodi idadi kubwa zaidi ya watoto waliokosa dozi za chanjo.

(RTRE, AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW