1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe: Mugabe apewa kinga

23 Novemba 2017

Mugabe atapewa ulinzi pamoja na familia yake nyumbani kwake Zimbabwe. Pia amehakikishiwa kuwa hatashitakiwa kwa makosa anayodaiwa kuyafanya wakati wa utawala wake wa kiimla uliodumu kwa miaka 37

Robert Mugabe und Grace Mugabe
Picha: Getty Images/J.Njikizana

Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robet Mugabe, pamoja na mke wake, Grace Mugabe, wataruhusiwa kuishi nchini humo bila kushitakiwa makosa waliyoyafanya. Hayo yamesemwa na msemaji wa chama tawala ZANU-PF. Wakati huohuo Uingereza imeutaka utawala mpya wa Zimbabwe kuweka wazi nia yao ya kuirejesha nchi katika mkondo wa demokrasia na wa maendeleo.

Msemaji wa chama  tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF, Simon Khaya Moyo, ameliambia shirika la habari la DPA kuwa Mugabe angali shujaa wa ukombozi anayeheshimiwa na kwamba alitekeleza mengi ya maendeleo kwa taifa wakati wa utawala wake.

Moyo amesema "Rais anayeondoka anafahamu vyema chuki ya umma dhidi ya mke wake na ghadhabu kutoka pande mbalimbali kuhusiana na jinsi alivyoshughulika na siasa za ZANU-PF. Kwa mantiki hiyo, ilikuwa muhimu kumpa uhakikisho kwamba familia yake yote, akiwemo mkewe, watakuwa salama." 

Kinga dhidi ya kushtakiwa

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe na mkewe Grace MugabePicha: Getty Images/J.Delay

Hatua ya kumpa Mugabe kinga imepokelewa vyema na baadhi ya watu, mmoja wao ni mkaazi wa Harare Munyaradzi Makosa: "Ninafikiri ni sawa kwamba rais wa zamani amepewa kinga kwa sababu amefanya mengi ya ukombozi wa nchi na japo alikosea mwisho mwisho, anastahili kinga."

Duru inayofahamu mazungumzo yaliyopelekea Mugabe kujiuzulu, imesema kuwa wamekubaliana kwamba kiongozi huyo atapewa ulinzi pamoja na familia yake nyumbani kwake na amehakikishiwa kuwa hatashitakiwa kwa makosa anayodaiwa kuyafanya wakati wa utawala wake wa kiimla uliodumu kwa miaka 37.

Mugabe hataki kuishi uhamishoni

Duru hiyo imeelezea kuwa Mugabe mwenye umri wa miaka 93 aliwaambia washauri kuwa anataka afe nchini Zimbabwe, hivyo hana mpango wa kuishi uhamishoni. Duru hiyo imeeeleza kuwa Mugabe aliyasema hayo kwa hisia nzito na kwa msisitizo.

Mugabe pia atapokea malipo ya kustaafu yatakayojumuisha fedha za kustaafu, za kulipia nyumba, marupurupu ya likizo na kusafiri, bima ya afya na ulinzi kamili.

Hayo yanafahamika wakati maandalizi ya kumuapisha Emmerson Mnangagwa kama rais kesho yakiendelea. Mnangagwa, aliyekuwa makamu wa rais wa Mugabe na pia kuwahi kuwa waziri wa sheria na ulinzi katika serikali ya Mugabe, alirejea nchini humo jana, tangu alipoondoka Zimbabwe alipofutwa kazi na Mugabe Novemba 6, kwa kile kilichoonekana kuwa ushindani kati yake na mkewe Mugabe, Grace, wa kukirithi kiti cha rais.

Emmerson MnangagwaPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Uingereza: Utawala mpya kuzingatia demokrasia na maendeleo

Katika tukio jingine, Uingereza imeutaka utawala mpya wa Zimbabwe kuweka wazi nia yao ya kuirejesha nchi katika mkondo wa demokrasia na wa maendeleo baada ya mwisho wa Mugabe. Waziri wa Masuala ya Afrika, Rory Stewart, amesema hayo alipowasili mjini Harare akiongeza kuwa matukio ya hivi karibuni yamewapa Wazimbabwe matumaini.

Mnangagwa aliye na umri wa miaka 75 angali amewekewa vikwazo na Marekani kuhusiana na matendo yake kama makamu wa Mugabe na mtekelezaji wa mikakati ya kiusalama. Aliwekewa vikwazo hivyo kufuatia kile Marekani ilichokiita kutekeleza ghasia na ukiukaji wa haki dhidi ya wapinzani wa kisiasa.

Alilaumiwa kwa kuongoza operesheni ya machafuko dhidi ya wapinzani wakati wa uchaguzi w arais mwaka 2008. Vikwazo hivyo pia vinamlenga Mugabe, mke wake na takriban maafisa 100 wa serikali na washirika wake.

Mwandishi: John Juma/DPAE/

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW