1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yaamuru bei kupandishwa

Josephat Charo22 Agosti 2007

Serikali ya Zimbabwe imewaamuru wafanyabiashara kuongeza bei za bidhaa muhimu ili kupunguza uhaba mkubwa uliosababishwa na hatua ya serikali kulazimisha bei zishushwe.

Maduka na bishara zilizoamriwa kupunguza bei zao miezi miwili iliyopita kama sehemu ya mkakati dhidi ya watu wanaolenga kujipatia faida kubwa uliozusha utata, sasa wataweza kuongeza bei za bidhaa zao kama vile sukari, mafuta ya kupikia, kuku na sabuni. Malipo kwa ajili ya huduma za simu pia yataongezeka kwa asilimia 20. Wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo wataweza kuongeza viwango wanavyowatoza wakulima kwa ajili ya mbegu za mahindi na dawa za kuua wadudu.

Mtalamu wa uchumi nchini Zimbabwe John Robertson anasema kushusha bei ya bidhaa kumesabisha matatizo makubwa nchini humo.

´Kwa sababu ya mabadiliko haya matatizo sasa yamezidi kuwa magumu. Hakuna bidhaa madukani. Watu hupigana ngumi madukani wakati sheheza za vyakula kama mkate zinapofika. Familia nyingi sana zinataabika kutokana na njaa. Wengi wanaishi na mlo mmoja kwa siku na hawana uhakika chakula kingine kitatoka wapi?´

Waziri wa viwanda wa Zimbabwe, Obert Mpofu, amesema anatambua umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu akisema juhudi zaidi zinatakiwa kufanywa kuongeza usafirishaji wa bidhaa katika soko. Wadau wote wanahimizwa kuwa na nia moja na mwelekeo unaolenga kuwanufaisha Wazimbabwe wote. Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Zimbabwe kuwaruhusu wafanyabiashara kuongeza bei za bidhaa zao, tangu ilipoanzisha operesheni iliojulikana kwa jina Dzikiza, iliyowalazimisha kupunguza bei za bidhaa.

Ingawa mwanzoni hatua hiyo ilishangiliwa kwa kuwa iliwawezesha Wazimbabwe kupata bidhaa ambazo hawakumudu kuzinunua, imesababisha upungufu mkubwa huku watengenezaji wa bidhaa hizo wakishindwa kukabiliana na gharama na utenganezaji wa bidhaa.

Mama huyu anayeishi katika mtaa mmoja wa madongo poromoka katika viunga vya mji mkuu Harare anaeleza hali ngumu inayomkabili.

´Mambo ni magumu kwangu kwa sababu siwezi kumudu hata kununua chakula. Hata watoto wangu wamekaa siku nyingi bila kunywa uji kwa kuwa bei ya sukari imepanda mno na sina pesa. Sifanyi kazi na mume wangu alikufa kitambo kwa hiyo naishi peke yangu nikijaribu kutafuta chakula hapa na pale. Siku nyengine nalazimika kuuza nguo zangu kwa kuwa sina cha kufanya kuwasaidia wanangu.´

Naibu kiongozi wa shirikisho la viwanda nchini zimbabwe, bwana Phillip Chigumira, amesema hatua mpya ya serikali ni nzuri kwa biashara na watumiaji wa bidhaa. Lakini mwanaume huyu ana maoni tofauti.

´Kwangu mimi mchakato huu wote hauna maana yoyote. Kwa sababu bidhaa muhimu zilizoshushwa bei hazimo madukani, hasa mkate. Unalazimika kuunga foleni kwa muda wa saa sita kabla kununua mkate mmoja tu. Hali imefikia pabaya na haiwezi kudhibitiwa. Hakuna cha kununua.´

´Tunaweza kuendelea katika mkondo huu kwa miaka mingi ijayo. Kwa vyovyote Zimbabwe haijakaribia kuanguka kabisa kiuchumi. Ukitaka kufahamu maana ya kuwa chini kabisa kiuchumi, unahitaji kuziangalia nchi kama Tanzania ilivyokuwa miaka 20 iliyopita, au Somalia ya sasa, ambayo iko nyuma sana kuliko sisi.´

Kwa sasa hakuna matumaini ya matatizo yanayoikabili Zimbabwe kupatiwa ufumbuzi hivi karibuni. Ukweli ni kwamba hali ngumu nchini humo inatarajiwa kuendelea.