zimbabwe yasherehekea mwa wa 27 wa Uhuru
18 Aprili 2007Zimbabwe leo imesherehekea miaka 27 ya Uhuru, huku Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo, akiushutumu upinzani kwa kile alichokiita ni kujaribu kuzusha vurugu na msukosuko. Katika hotuba yake kwenye uwanja wa michezo wa Harare, Mugabe mbali na kuushambulia upinzani na hasa kiongozi wa chama kikuu cha Movement for Democratic Change-MDC Morgan Tsvangirai, aliyashambulia madola ya kigeni na alielekea kuzilenga hasa Marekani na Uingereza.
Nchi hizo mbili zinaushutumu vikali utawala wake kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, tangu uchaguzi wa Rais 2002, ambao umetajwa kuwa ulijaa mizengwe na udanganyifu.
Katika hotuba yake hiyo leo, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 83 alisema hivi karibuni kumeshuhudiwa jaribio la baadhi ya wapinzani waliopotoshwa kutaka kuzusha msukosuko, na akaongeaza kwamba ujumbe wa serikali yake unabakie kuwa ule ule : kamwe haitosita kupambana na watu wa aina hiyo.
Kiongozi huyo aliye madarakani tangu uhuru kutoka kwa Uingereza April 18, 1980 alizipinga hoja za kwamba havumilii upinzani , akisema upinzani una kila nafasi ya kuendesha shughuli zake, ili mradi tu hayo yanafanyika chini ya misingi ya kuheshimu sheria.
Akamshambulia tena kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai akisema ni kibaraka , anayetumiwa na Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair na Rais George W. Bush wa Marekani, kama sehemu ya kile kinachoitwa kampeni ya kuleta mabadiliko ya utawala Zimbabwe.
Rais Mugabe alisema wanachotafautiana na Tsvangirai ni kuwa anakubali wanachosema Bush na Blair kwamba uchaguzi wa 2002 haukua halali, lakini mwenyewe Tsvangirai hana fikra za kuboresha hali za maisha ya umma wa nchi hiyo, akiongeza “ kile anachokipigia debe tu ni kwamba Mugabe lazima angoke madarakani.” Wakati akizungumza hayo, wafauasi wake uwanjani walikua wakipiga kelele Gushungo, Gushungo jina la ukoo wa Mugabe
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Makamu wa Rais Joyce Njuru ambaye kawa mujibu wa uvumi uliozagaa ni miongoni mwa wanaowania nafasi ya Mugabe pindi akistaafu, Lakini Viongozi wa taifa kutoka nchi nyengine za kusini mwa Afrika hawakuonekana na haikuweza kufahamika kama walialikwa katika sherehe hizo za miaka 27 ya uhuru wa Zimababwe au la .
Kiongozi wa MDC Tsvangirai pia hakuhudhuria na maafisa wa chama chake walisema “ hakuna cha kusherehekea .”