1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yatangaza ukame kuwa janga la kitaifa

4 Aprili 2024

Zimbabwe imeungana na Zambia na Malawi kutangaza ukame kuwa janga. Katika taarifa iliyotolewa na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema nchi yake inahitaji zaidi ya dola bilioni mbili kukabiliana na njaa

Zimbabwe
Mazao nchini Zimbabwe yameharibika kufuatia ukame unaoikumba nchi hiyoPicha: Privilege Musvanhiri/DW

Zimbabwe imetangaza ukame kuwa janga la kitaifa. Katika taarifa iliyotolewa na rais, Emmerson Mnangagwa, nchi hiyo inahitaji zaidi ya dola bilioni mbili kwa ajili ya kuwasaidia raia wa nchi hiyo wanaokabiliwa na njaa.

Tangazo hilo linafuatia matangazo kama hayo yaliyotolewa mwezi Februari na mwanzoni mwa mwezi Machi na mataifa jirani ya Zambia na Malawi, wakati ukame uliosababishwa na hali ya El Nino inayoikumba dunia ukiendelea kuleta mzozo wa kibinadamu kusini mwa Afrika.

Soma zaidi. Zimbabwe yatangaza ukame nchini humo kuwa janga la taifa

Hali hiyo sasa imeteketeza mazao na kuacha mamilioni ya watu katika nchi hizo wakiwa kwenye hitaji kubwa la msaada wa haraka wa chakula.

Katika hotuba yake, Rais Mnangagwa ametaja kuwa asilimia 80 ya eneo la nchi hiyo lilikabiliwa na upungufu mkubwa wa mvua na ametolea mwito jumuiya ya kimataifa kuisadia nchi hiyo na msaada wa chakula.

Shirika la misaada la Marekani USAID tayari limeanza mpango wa kuwasaidia watu milioni 2.7 wanaokabiliwa na njaa nchini ZimbabwePicha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP Photo/picture alliance

Shirika la Mpango wa chakula Duniani WFP tayari limekwisha anzisha mpango wa msaada wa chakula unaolenga kuwafikia watu milioni 2.7 wanaokabiliwa na njaa nchini Zimbabwe sawa na kusema kuwa ni asilimia 20 ya idadi ya watu nchini humo ndio watakaopatiwa msaada huo

Soma zaidi. Wakulima wakabiliwa na ukame Kusini mwa Jangwa la Sahara

Akipokea msaada wa chakula, Zanyiwe Ncube ambaye ni mkazi wa Mangwe, Zimbabwe amesema kwa sasa hali ya chakula ni mbaya mnoo.

“Hali yetu ya chakula ni ngumu, tunakula mara moja tu kwa siku, kwa sababu hatuna kitu shambani, hata punje moja. Kila kitu kimekauka kwa ukame. Pia tuna matatizo ya kutafuta maji. Tunaomba kwamba watu watusaidie kwa maji kama wataweza hata kutuchimbia kisima." amesema Zanyiwe.

Hali ya huduma ya msingi ni ngumu

Zaidi ya asilimia 60 ya watu milioni 15 wa Zimbabwe wanaishi vijijini wakifanya shughuli za kilimo wanachokitumia kama mhimili mkuu wa kuendesha maisha yao na kwa hali ilivyo kwa sasa mambo ni magumu zaidi na itakuwa ni vigumu hata kuhimili kulipia gharama za msingi za kuendesha maisha yao.

Soma zaidi. Asilimia 44 ya mazao ya mahindi nchini Malawi yameathirika na ukame

Tamko la Mnangagwa litafungua njia kwa mashirika ya misaada kulisaidia taifa hilo la kusini mwa Afrika ingawa ipo hofu kuwa misaada itakoyotolewa inaweza kutowafikia watu wote kulingana na upungufu wa rasilimali na mizozo inayoendelea duniani.

Zaidi ya watu milioni 2.7 wanakabiliwa na njaa nchini ZimbabwePicha: Privilege Musvanhiri/DW

Kwa upande mwingine, taifa jirani la Zambia lilitangaza kuwa karibu nusu ya mazao nchini humo yameharibika na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuisaidia kukabiliana na njaa.

Huko Malawi pia Rais wa nchi hiyo Lazarus Chakwera alitangaza hivi karibuni kwamba nchi yake inahitaji msaada wa zaidi ya dola milioni 200 kukabiliana na janga la ukame linalozikumba wilaya zake 23 kati ya 28 za nchi hiyo.

Shirika la Misaada la Marekani, USAID, linakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 20 walioko kusini mwa bara la Afrika wapo kwenye uhitaji mkubwa wa msaada wa haraka wa chakula.