Zimbabwe yazindua noti mpya.
12 Desemba 2008Benki kuu nchini Zimbabwe imeanzisha matumizi ya noti ya dolla millioni 500, huku taifa hilo likikabiliwa na mfumuko mkubwa kabisa wa bei duniani na upungufu wa sarafu.Noti hiyo ya nusu billioni ni dola 10 za marekani.Benki ya dunia imesema ilichukua hatua hiyo ili kuwarahisia wazimbabwe mzigo wa pesa.
Noti hiyo ya nusu billioni yenye thamani ya dola 10 za marekani ilitolewa sambamba na nyingine ya dolla millioni 200. Waziri wa fedha alitangaza matumizi ya noti hizo katika gazeti la serikali, na hivyo kufikisha 29 idadi ya noti mpya ambazo zimeanza kutumiwa mwaka huu.
Ni alhamisi iliyopita tu Zimbabwe ilizindua noti nyingine ya dolla millioni 100 wakati huo ikiwa na thamani ya dolla 14 za marekani. Wiki moja baadaye noti hiyo ni ya thamani chini ya centi 50.
Mfumuko wa bei nchini Zimbabwe ulikadiriwa mwezi Julai kuwa asilimia millioni 231, lakini hivi sasa unaaminika kuwa zaidi ya asilimia hiyo. Benki kuu nchini Zimbabwe imeendelea kujikakamua kuchapisha noti mpya kwa haraka ili kulingana kasi ya kupanda bei kwa bidhaa mara kadhaa kwa siku.
Kutokana na upungufu wa sarafu, Wazimbabwe wanaruhusiwa kutoa pesa zao kutoka benki mara moja kwa wiki, Mzimbabwe wa kawaida akiruhusiwa dolla millioni 500 huku makampuni yakiruhusiwa kutoa dolla millioni 50 pekee.
Foleni ndefu zimekuwa jambo la kawaida katika mabenki, huku watu wakisubiri kwa masaa mengi kutoa pesa, ambazo wakati mwingine haziwatoshi kwa siku. Wengine hata wamelazimika kupiga kambi usiku kucha katika mabenki ili kuwa wa kwanza kutoa pesa siku inayofwata.
Wakati Zimbabwe ikikabiliwa pia na upungu wa chakula, ugonjwa wa kipundupindu ulizuka Agosti mwaka huu unakisiwa kuwaua karibu watu 800. Akizungumza wakati wa mazishi ya mfuasi mmoja mkuu wa chama tawala nchini humo cha ZANU-PF rais Robert Mugabe alisema mashirika ya kutoa misaada kwa ushirikiano na madaktari nchini Zimbabwe yameudhibiti ugonjwa huo.
"Kwa sababu ya kipundupindu, bw Brown anataka nguvu za kijeshi zitumike chini Zimbabwe, Sarkozy, na pia Bush wanataka nguvu za kijeshi zitumike nchini Zimbabwe. Lakini nina furaha kuwa madaktari wetu wakisadiwa na wengine kutoka shirika la WHO, hivi sasa wamekabiliana na ugonjwa huo .Kwa hivyo kwa kuwa hivi sasa hakuna kipindupindu hakuna haja ya vita tena. Wacha tuwambia kuwa kipindu pindu hakipo tena."
Rais Mugabe amekuwa akiishtumu marekani na uingereza kwa kujaribu kutafuta kuungwa mkono na mataifa mengine ya magharibi kuipindua serikali yake kutokana na kuzuka kwa ugonjwa huo wa kipindupindu.
Mashirika ya Umoja wa mataifa yanayotoa misaada nchini Zimbabwe, yameonya kuwa idadi ya watu watakaombukizwa ugonjwa huo huenda ikafikia elfu 60 iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa katika muda wa wiki chache zijazo.
Hospitali nyingi zimefungwa nchini Zimbabwe kutokana na ukosefu wa dawa na vifaa,hatua ambayo imewalazimisha baadhi yao kutafuta matibabu katika nchi jirani ya Afrika kusini. Kwa mujibu wa maafisa wa afya nchini afrka kusini wamepokea karibu wagonjwa 700 wa kipindupindu.