Zoé Kabila apinga kuvuliwa ubunge Kongo
26 Agosti 2022Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Wizara ya Mipango ya Miji na Makaazi ilimlazimisha aondoke na kuacha mali ya serikali aliyoambiwa ameivamia kinyume na sheria huko Kinshasa. Hata hivyo, kampuni ya uchimbaji ya madini ya Katanga Premier, ambayo Zoé Kabila ni mshirika, inadai kuwa mmiliki wa nyumba hiyo.
Imetimu miezi kadhaa tangu serikali ya Kongo kuanza operesheni ya kurejesha mali isiyohamishika ya serikali. Lakini mawakili wa Zoé Kabila wanaamini kuwa nyumba iliyo katika wilaya ya Gombe hapa mjini Kinshasa haijahusika kwani ni ya kampuni ya madini ya Katanga Premier, ambayo ni mnunuzi wa nne baada ya wamiliki kadhaa. Benjamin Lukamba, mmoja wa mawakili hao, anashutumu kufukuzwa kinyume cha sheria: "Sisi tunayo hatimiliki, tunawezaje basi kufukuzwa? Hakuna hatua ya mahakama inayoondoa mamlaka ya cheti cha usajili. Nyumba hii siyo tena ya serikali, na hivyo, tumechukua hatua za kisheria ili kukomesha usumbufu, na pia hatua za kiutawala."
Matamshi hayo yamekanushwa na Wizara ya Mipango ya Miji na Makaazi hapa Kongo, ikisisitiza kwamba hakuna mtu anayeweza kudai kuwa amepata mali isiyohamishika ya serikali bila amri ya kufutwa, kama anavyoeleza Célé Kanangila, mkuu wa ofisi ya Pius Mwabilu, Waziri wa Mipango ya Miji na Makaazi:
"Wanataja cheti cha usajili huku wakipuuza utaratibu na njia za kuingia katika umiliki wa mali isiyohamishika ya serikali. Hati muhimu inayohitajika ni agizo la kufuta. Serikali lazima kwanza ifute nyumba yake kutoka mali yake binafsi. Ikiwa hakuna amri hiyo, basi huu ni wizi."
Lakini mawakili wa Zoé Kabila wanakumbusha kuwa nyumba hiyo ilitolewa mwaka 1989 na Rais Joseph-Désiré Mobutu kwa mwendesha mashtaka mkuu wa zamani wa jeshi. Kisha ilinunuliwa na wamiliki kadhaa kabla ya Katanga Premier kuwa mnunuzi wa nne.
Mwandishi: Jean Noël Ba-Mweze/DW Kinshasa