Zoezi la kuhesabu kura juu ya katiba mpya linaendelea Chad
18 Desemba 2023Ishara zote zinaonyesha kuwa katiba mpya itaidhinishwa na kufungua njia kuelekea kufanyika kwa uchaguzi na hivyo basi kurudi kwa utawala wa kiraia.
Hata hivyo, idadi kubwa ya wapinzani na mashirika ya kiraia katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati yalitoa wito kwa wananchi kususia kura hiyo ya jana Jumapili.
Upinzani unaeleza kuwa, kura hiyo imeandaliwa kama mbinu ya kumfungulia njia rais wa sasa wa mpito Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno kuendelea kusalia madarakani na kuendeleza siasa za "urithi" zilizoanzishwa na marehemu babake miaka 33 iliyopita aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi.
Kambi ya "ndio" inaonekana kuwa na uhakika wa ushindi baada ya kampeni ilivyofadhiliwa na utawala wa kijeshi dhidi ya upinzani uliogawanyika na ambao wanachama wake wamekamatwa na kukabiliwa na vitisho vya mara kwa mara.