Watanzania wanasubiri matokeo ya uchaguzi mkuu
26 Oktoba 2015Watanzania wanasubiri kwa shauku matokea ya uchaguzi mkuu uliyofanyika hapo jana, ambao unatajwa kuwa wa ushindani zaidi katika historia ya nchi hiyo. Mgombea wa chama tawala - chama cha Mapinduzi CCM, anachuana vikali na mgombea wa muungano wa upinzani Edward Lowassa, ambaye alielezea wasiwasi kuwa huenda uchaguzi huo usiwe huru na wa haki.
Jana jioni chama cha Chadema, ambacho ni sehemu ya muungano wa upinzani unaoongozwa na Lowassa, kilisema polisi ilivamia kituo chake kujumlisha kura jijini Dar es Salaam na kuwakamata maafisa wa upinzani.
Mvutano wowote juu ya matokeo ya uchaguzi huo, unaotajwa kuwa wenye ushindani mkali zaidi tangu Tanzania ilipojipatia uhuru wake - unaweza kuongeza hali ya wasiwasi katika taifa ambalo limekuwa na utulivu kiasi tangu kumalizika kwa ukoloni wa Kiingereza mwaka 1961.
Baadhi ya maafisa na wachambuzi wameelezea wasiwasi hasa kuhusu mivutano katika visiwa vinavyojitawala vya Zanzibar, ambako wapinzani waliituhumu serikali kwa kuwafanyia vitisho kuelekea uchaguzi huo.
Lakini kwa ujumla zoezi la uchaguzi limepita salama nchini kote, ambako uhuhduriaji umekuwa mkubwa hasa katika maeneo ya mijini, hali iliyosababisha ucheleweshaji. Utafiti wa maoni na wachambuzi wamebashiri ushindi kw amgombea wa chama tawala John Magufuli, lakini wengi wanatarajia wingi wa wabunge kiliyojivunia chama hicho kupungua pakubwa.
Chama cha CCM kilichoko madarakani kwa zaidi ya nusu karne, kimekabiliwa na shinikizo kuongeza kasi ya maendeleo ya rasilimali muhimu za taifa hilo ili kuchochea ukuaji wa kiuchumi, na kupungua viwango vikubwa vya umaskini.
Karibu watu milioni 22.75 walijiandikisha kupiga kura, ambapo karibu asilimia 53 ya idadi hiyo wana umri wa miaka 35 na kwenda chini. Katika vituo vingi vy akupigia kura, CCM na wapinzani walipeleka wasimamizi wao, ambapo kila mmoja alituma matokeo katika vituo vyao vya kujumlisha, ili kupata kujua mwelekeo wa matokeo, na kujaribu kuzuwia wizi wa kura.
Mwenyekiti wa taifa wa Chadema Freeman Mbowe, alisem Polisi ilivamia kituo chao cha kujumlisha kura na kuonyesha kuwa serikali ya CCM ilikuwa inatumia mbinu za kidikteta kubadili matokeo ya kura na kuwatisha watu.
Wasemaji wa serikali na hata jeshi la polisi hawakuweza kupatikana na shirika la reuters kuzungumzia tuhumu hizo za Chadema.
Siku moja kabla ya zoezi la kupiga kura, Lowassa, ambaye alijindoa kwenye chama tawala mwezi Julai, baada ya chama hicho kumnyima fursa ya kukiwakilisha katika uchaguzi huu, alisema atakubali tu kushindwa ikiwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki. "Iwapo hautakuwa hivyo, sintokubali," alisema.
Rais anaemaliza muda wake Jakaya Kikwete, ambaye atastaafu baada ya kumaliza mihula yake miwili anayoruhusiwa kikatiba, alitoa wito wa kujiepusha na vurugu, na kuonya kuwa yeyote atakaesababbisga vurugu atakiona cha moto.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kuanza asubuhi ya leo, na tume ya uchaguzi ilisema inapanga kumtangaza mshindi katika muda wa siku tatu tangu kumalizika kwa upigaji kura.
Magufuli na Lowassa wote wamewavutia maelfu ya watu kwenye mikutano yao, wakiahidi kukomesha mgawo wa mara kwa mara wa umeme, na kuhakikisha ukuaji wa kiuchumi unawafikia watu maskini.
Pia wameahidi kupambana na rushwa iliyokithiri, kujenga barabara na kuboresha miundombinu iliyochakaa, ambayo inazidisha ugumu katika maisha ya kila siku.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.
Mhariri: Sekione Kitojo