Zoezi la kuhesabu kura linaendelea Ufilipino
9 Mei 2022Takriban miaka 40 baada ya baba yake na wajina wake kuondolewa madarakani kufuatia maandamano ya umma yaliyosababisha pia familia yake kukimbilia uhamishoni, Marcos Jr anakaribia kukamilisha azma ya kuurejesha ukoo huo katika kilele cha mamlaka ya kisiasa.
Wagombea 10 wanawania kumrithi Rais Rodrigo Duterte katika uchaguzi unaoonekana na wengi kama wakati muhimu kwa demokrasia dhaifu ya Ufilipino. Lakini ni Marcos Jr pekee na mpinzani wake Leni Robredo, makamu wa rais aliyeko madarakani, ndio wenye nafasi ya kushinda.
Mapema asubuhi Jumatatu, wapiga kura waliovalia vinyago walipanga foleni ndefu kupiga kura zao katika vituo 70,000 vya kupigia kura katika visiwa hivyo.
Maafisa wa uchaguzi wamesema, vituo vya kupigia kura vilifungwa rasmi saa moja usiku Jumatatu, lakini wapiga kura walio ndani ya mita 30 kutoka eneo hilo bado waliruhusiwa kupiga kura. Mbwa wa kunusa mabomu walizunguka katika kituo cha kupigia kura kabla ya Marcos Jr kuwasili akiwa na mdogo wake wa kike, Irene na mwanawe mkubwa Sandro.
Sandro, mwenye umri wa miaka 28, ambaye anawania kwa mara ya kwanza nafasi katika bunge la wilaya kwenye jimbo la Ilocos Norte, amekiri kuwa historia ya familia hiyo ni "mzigo", lakini aliongeza: "Ni moja ya jambo tunalojaribu kuliendeleza na kulilinda na ni bora zaidi tunapohudumu."
Wapiga kura kuongezeka
Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilitarajiwa kuwa juu miongoni mwa zaidi ya Wafilipino milioni 65 waliotimiza umri wa kupiga kura.
"Tunaweza kusema kwamba uchaguzi wetu ni wa mafanikio kutokana na watu wengi waliotikia kupiga kura," alisema George Garcia kutoka Tume ya Uchaguzi.
Baada ya kampeni kali, kura za maoni zilionyesha kuwa Marcos Jr anaelekea kupata ushindi wa kishindo. Nchini Ufilipino, mshindi lazima apate kura nyingi zaidi kuliko wapinzani wake.
Tangu Robredo atangaze azma yake ya kugombea nafasi hiyo ya juu mwezi Oktoba, vikundi vya watu wa kujitolea vimeongezeka kote nchini vikijaribu kuwashawishi wapiga kura kumuunga mkono katika kile wanachokiona kama vita kwa ajili ya kuuokoa uhai wa nchi.
Baada ya miaka sita ya utawala wa kimabavu wa Duterte, wanaharakati wa haki, viongozi wa Kanisa Katoliki na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanahofia kwamba Marcos Jr atapata ujasiri wa kutawala kwa mkono wa chuma iwapo atashinda kwa kura nyingi.
Mazoea ya badhi ya koo kusalia madarakani Ufilipino
Robredo, mwanasheria na mwanauchumi mwenye umri wa miaka 57, ameahidi kuusafisha mfumo mchafu wa siasa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukiikumba demokrasia mbovu nchini humo, ambapo majina machache ya ukoo fulani ndio yenye kutawala.
Marcos Jr na mgombea mwenza Sara Duterte, wote wakiwa watoto wa viongozi wa kimabavu, wamesisitiza kuwa wana sifa bora zaidi ya "kuiunganisha" nchi, ingawa maana ya kauli hiyo haifahamiki.
Maelfu ya wafuasi waliovalia mavazi mekundu walijitokeza katika mikutano ya Marcos Jr na Duterte mjini Manila siku ya Jumamosi, walipokuwa wakifanya kapeni zao za mwisho. Josephine Llorca amesema serikali zilizofuatana nchini Ufilipino tangu mapinduzi ya mwaka 1986 yaliyoiondoa familia hiyo, zimeshindwa kuboresha maisha ya watu maskini.
Soma zaidi: Ufilipino yapandisha umri wa ridhaa ya ngono kuwa miaka 16
Wagombea wengine wanaowania kiti cha urais ni pamoja na gwiji wa ndondi Manny Pacquiao na aliyekuwa mwigizaji wa barabarani aliyegeuka kuwa mwigizaji Francisco Domagoso. Haiba badala ya sera kwa kawaida huathiri uchaguzi kwa watu wengi ingawa hongo za kununua kura na vitisho pia ni matatizo ya kudumu katika chaguzi za Ufilipino.
(AFP, Reuters)