1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuwahamisha watu kutoka Afghanistan bado ni gumu

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
22 Agosti 2021

Muda unazidi kuibana Marekani na washirika wake wakati ambapo wanaendelea na juhudi za kuwaondoa watu kutoka nchini Afghanistan. Zoezi hilo linazidi kuwa gumu huku tahadhari zikiendelea kutolewa.

Afghanistan I Evakuierung am Flughafen Hamid Karzai
Picha: Mark Andries/US MARINE CORPS7AFP

Umoja wa Ulaya umeelezea kwamba huenda itakuwa vigumu kuwasafirisha watu wote kwa wakati uliokusudiwa. Marekani inalenga Agosti 31 kuwa siku ya mwisho ya kuwahamisha watu kutoka Afghanistan lakini mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema mipango ya kuwahamisha watu 60,000 katika kipindi hicho kifupi haiwezekani.

Siku sita tangu kundi la wanamgambo wa Taliban lilipochukua udhibiti nchini Afghanistan, maelfu ya watu wanajaribu kuondoka kutoka nchini humo katika operesheni ngumu ya kuwahamisha watu katika historia ya miaka ya karibuni.

Raia wa Afghanistan nje ya uwanja wa ndege wa Hamid Karzai mjini KabulPicha: Haroon Sabawoon/AA/picture alliance

Picha na mikanda ya video zaonesha misongamano ya watu kwenye viunga vya uwanja wa ndege mjini Kabul, kitovu cha operesheni hiyo ya kuwaondoa watu inayoendeshwa kwa sehemu kubwa chini ya usimamizi wa Marekani.

Kutokana na hali hiyo ya misongamano mikubwa Marekani na Ujerumani zimewataka raia wake kuepuka eneo hilo la uwanja wa ndege kwa hofu kwamba hali ya usalama inaweza kuwa hatarishi.

Wakati huohuo lawama zinatolewa kutoka pande mbalimbali kuhusiana na hali ya Afghanistan. Rais wa Marekani Joe Biden anakabiliwa na ukosoaji unaoongezeka kutokana na video zinazoonyesha vurugu za mara kwa mara nje ya uwanja wa ndege wa Kabul na pia Waafghanistan waliojawa na hofu ya kushambuliwa na Taliban wakiomba wasiachwe nyuma katika zoezi la kuwaondoa watu kutona nchini mwao.

Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Katika mahojiano ya kipekee na DW, kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha kisoshalisti cha mrengo wa kushoto Die Linke, Janine Wissler amekosoa vikali hatua ya serikali ya Ujerumani kuhusu Afghanistan. Amesema imehatarisha maisha ya wanadamu.

Janine Wissler, ameiambia DW kuwa serikali ya Ujerumani imekosea kusimamisha kabisa misaada ya maendeleo kwa Afghanistan baada ya Taliban kuchukua madaraka nchini humo. Amesema licha ya hali hiyo sasa sio wakati wa Ujerumani kuondoa misaada ya maendeleo kwa watu wa Afghanistan.

Wataliban mjini KabulPicha: Abdullah Abdullah/Handout/REUTERS

Wakati huo huo baadhi ya viongozi wakuu wa Taliban wanakutana mjini Kabul kujadili juu ya kuunda serikali mpya ya Afghanistan miongoni mwao ni pamoja na mwakilishi kutoka mtandao wa Haqqani wa wanamgambo wanaoogopwa zaidi nchini humo.

Wahaqqani wamelaumiwa kwa kufanya baadhi ya mashambulio mabaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni, yaliyosababisha vifo vya raia wa Afghanistan, maafisa wa serikali na wanajeshi wa vikosi vya kigeni. Lakini wanatarajiwa kuwa washirika wenye nguvu katika utawala mpya baada ya Taliban kutwaa mamlaka ya Afghanistan wiki iliyopita.

Vyanzo:/RTRE/AP/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW