Zoezi la Sudan ya Kusini lasifiwa
18 Januari 2011Wiki iliyopita, kiasi ya watu milioni nne katika Sudan ya Kusini walipiga kura kuamua iwapo eneo hilo lenye utajiri wa mafuta, lijitenge na Kaskazini. Licha ya kuwepo vitisho vya mashambulio na harakati za kutayarisha kura hiyo ya maoni kuendelea hadi dakika ya mwisho, zoezi hilo lilifanyika kwa amani kinyume na vile ilivyotazamiwa na baadhi ya wachambuzi. Kwa mujibu wa wasimamizi wa kimataifa, kura hiyo ya maoni, kwa sehemu kubwa, ilikwenda kwa usalama. Takriban vituo vyote vya kupigia kura vilikuwa na orodha ya wapiga kura na karatasi za kupigia kura. Maafisa wa uchaguzi pia wamesifiwa kwa kazi nzuri iliyofanywa, lakini kulishuhudiwa pia vitendo vya kuwatisha wapiga kura.
Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika baadhi ya maeneo ya Sudan ya Kusini ilipindukia asilimia 90. Hiyo ni zaidi ya kiwango cha asilimia 60 kinachohitajiwa ili matokeo ya kura ya maoni yaweze kutambuliwa. Lakini katika kaskazini mwa nchi, ambako wananchi wenye asili ya Sudan ya Kusini walikuwa pia na haki ya kupiga kura, ni wachache walioitumia fursa hiyo. Josef Sayer, mkurugenzi mkuu mtendaji wa shirika la misaada la Kijerumani Misereor alikuwa msimamizi mmojawapo. Anasema, watu walihofia kwamba walikuwa wakitazamwa na vikosi vya usalama. Vile vile hawakuwa na hakika iwapo kura zao zitahesabiwa.
Kwa upande mwingine, Abyei ni eneo linaloendelea kuwatia wasiwasi wasismamizi hao wa kimataifa. Wakaazi wa wilaya hiyo iliyopo kati ya mpaka wa Sudan ya Kaskazini na Sudan ya Kusini, walikuwa wapige kura ya maoni katika zoezi maalum kuamua iwapo wabakie na kaskazini au wajiunge na kusini. Lakini kura hiyo imeahirishwa kwa muda usiojulikana kwa sababu ya mzozo wa kisiasa. Eneo hilo linagombewa na kila upande kwa sababu ya utajiri wake mkubwa wa mafuta. Kwa maoni ya wasimamizi Sudan ya Kusini haitoweza kuunda taifa huru kwa usalama ikiwa hatima ya Abyei haitoamuliwa. Mjumbe wa Umoja wa Ulaya, Veronique de Kayser, amesema:
"Kwa hakika suala la Abyei ndio ufunguo unaowaeza kufungua mlango kwa matatizo mengine. Kwa hivyo, ni lazima litatuliwe katika kiwango cha kisiasa, tena kwa kipaumbele cha juu kabisa. kwani linaweza kusambaratisha eneo zima, ikiwa suluhisho la kisiasa halitopatikana haraka."
Majadiliano kuhusu eneo hilo tajiri la Abyei bado hayakuanza, lakini kura zilizopigwa Sudan ya Kusini zimeshaanza kuhesabiwa. Matokeo ya mwanzo kutoka Juba, mji mkuu wa kusini, yanaonyesha kuwa idadi kubwa ya wakaazi wa eneo hilo wanataka uhuru. Matokeo ya mwisho yanatazamiwa mwezi wa February.
Mwandishi: Pelz, Daniel/ZPR
Mpitiaji:Miraji Othman