1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuckerberg aomba msamaha na kuapa kurekebisha mambo

23 Mei 2018

Mkurugenzi wa Facebook Mark Zuckerberg ameomba msamaha kwenye Bunge la Ulaya kutokana na madhara yaliyosababishwa na kuvuja kwa data za watumiaji wa mtandao huo na pia kwa kushindwa kupambana na habari za bandia. 

Brüssel EU-Parlament | Mark Zuckerberg, Facebook-CEO
Picha: picture-alliance/AA/European Parliament

Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg aliomba msamaha kwa watumiaji wa Ulaya wa mitandao ya kijamii na kuahidi kupambana na habari za bandia na vile vile ameahidi kwamba data za watumiaji hao zitalindwa vyema. 

Zuckerberg alifika mbele ya viongozi wa makundi ya kisiasa wa Bunge la Ulaya baada ya Facebook kukubali kwamba ilitoa taarifa binafsi za watumiaji wapatao milioni 87 kwa kampuni ya Cambridge Analytica ya nchini Uingereza, zikiwemo zile za watumiaji karibu milioni 2.7 kutoka kwenye nchi za Umoja wa Ulaya. Facebook ilikubali kwamba ilitoa taarifa hizo binafsi kwa njia isiyo sawa.

Katikati Mark Zuckerberg akijibu maswali ya wabunge mjini Brussels Picha: Reuters/Reuters TV

hata hivyo Zuckerberg aliyakwepa baadhi ya maswali magumu aliyoulizwa na wabunge hao, na kisha kuomba msamaha kutokana na sera za Facebook zilizorahisisha kuenea kwa habari bandia wakati wa uchaguzi wa rais wa Marekani wa 2016 na pia katika matokeo ya kura ya maoni juu ya Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa Ulaya hata hivyo wamelalamika kwamba Zuckerberg hakutoa majibu halisi juu ya matumizi mabaya ya data za mamilioni ya watumiaji wa mtandao huo. Jan Philipp Albrecht, mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia ulinzi wa data za Umoja huo (GDPR) amesema ipo haja ya kuwepo ulinzi mkubwa.

Mjumbe huyo maalum anayeshughulikia masuala ya ulinzi wa data katika Umoja wa Ulaya amesema pia uangalizi unahitajika zaidi kwenye shughuli za mtandao huo wa Facebook, kwa mfano katika kuitenganisha Facebook na WhatsApp au Facebook Messenger ambapo hatua kama hiyo sasa itakuwa ni chaguo la mtu binafsi baada ya usiku wa leo. Bwana Albrecht amesema hilo ni moja kati ya maswali ambapo Mark Zuckerberg hakutoa majibu ya kina.

Rais wa bunge la Ulaya Antonio TajaniPicha: DW/B. Wesel

Zuckerberg ameomba msamaha kwa niaba ya kampuni yake kwa kushindwa kuzuia kutumiwa vibaya baadhi ya mifumo yake ya internet huku wengi wa wabunge waliokuwepo katika mahojiano hayo wakisema bilionea huyo wa Facebook alishindwa kutoa majibu yaliyoweza kuwatoa wasiwasi walio nao.

Mfumo wa kujibu maswali ulimruhusu Zuckerberg kujibu maswali hayo mwishoni, na hivyo kuwaacha wabunge wakiwa wamekata tamaa kutokana kushindwa kupata majibu ya moja kwa moja kwa maswali yao.

Rais wa Bunge la Ulaya Antonio Tajani alimwambia Zuckerberg kwamba kufika kwake kumetoa ishara muhimu ya heshima  wake kwa Bunge hilo pamoja na wananchi wa Ulaya.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPA

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW