1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma aibashiria ushindi ANC

Admin.WagnerD6 Mei 2014

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amekibashiria ushindi chama tawala cha ANC katika uchaguzi wa Jumatano, na kuongeza kuwa ikiwa atachaguliwa tena, serikali yake itaboresha maisha ya watu maskini .

Wahlen Südafrika 2014
Picha: picture-alliance/dpa

Watu wapatao 50000 ambao wanaishi katika maeneo yanayokaliwa na watu maskini, waliandamana hapo jana wakiishinikiza serikali kutoa huduma bora katika eneo la Nsuze lililopo katika jimbo la Kwazulu Natal.

Kwa mujibu wa jeshi la polisi la nchi hiyo hakuna ambaye alijeruhiwa lakini waandamanaji 40 walikamatwa na polisi kutokana na maandamano hayo.

Akiongea na waandishi wa habari, Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma ameahidi kama atachaguliwa kuendelea kuingoza nchi hiyo kwa kipindi kingine ataongeza kasi ya kuboresha miundombinu ya maeneo hayo yanayokaliwa na maskini.

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance Helen Zille wakimsubiri kuwahutubia.Picha: Reuters

Aishtumu AMCU kwa vurugu

Katika mkutano huo, Rais Zuma pia amekishutumu chama cha wachimbaji Madini na Ujenzi cha nchi hiyo (AMCU) kwa kushindwa kuwajibika huku kikiendesha maandamano ya kudai mishahara kwa kipindi cha miezi minne hali ambayo Rais Zuma anasema ilisababisha kuwepo kwa wasiwasi wa baadhi ya wafanyakazi kupoteza ajira zao kutokana na vurugu hizo.

"Chama cha wafanyakazi kinawajibu wa kuhakikisha wafanyakazi wanalindwa hivyo hawapotezi ajira zao, hauwezi kuitisha maandamano ambayo yatasababisha wafanyakazi kupoteza ajira zao" Alisema Rais Zuma katika mkutano huo.

Aidha Rais Zuma amekanusha kuhusika na ufisadi wa kutumia zaidi ya dola millioni 20 kwa ajili ya kukarabati nyumba yake binafsi iliyopo Nkandla.

Apuuza tuhuma za ubadhirifu dhidi yake

Ripoti iliyotolewa na shirika linalohusika na udhibiti wa mali za umma, ilimtuhumu Rais Zuma kutumia kiasi hicho kwa ukarabati wa kuimarisha ulinzi wa nyumba yake hiyo lakini mwenyewe anasema ripoti hiyo haikutoa ushahidi wa kutosha ambao unaonesha alitumia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya maslahi yake binafsi.

Bango la kampeni ya chama cha ANC na mgombea wake mkuu rais Jacob Zuma.Picha: Reuters

Chama kikubwa cha upinzani nchini Afrika Kusini, Democratic Alliance kimesema ni kweli Rais Zuma anahitaji ulinzi, lakini kiasi hicho kilichotumika kilikuwa ni kikubwa mno.

Rais Zuma anatarajia kupiga kura katika eneo ambalo makazi yake binafsi yapo la kwa-Nxamalala, Nkandla, KwaZulu-Natal.

Uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unatarajia kufanyika hapo kesho ambapo mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya chama tawala cha ANC kinachoongozwa na Rais Jacob Zuma na kile kikubwa cha upinzani cha Democratic Alliance.

Mwandishi: Anuary Mkama/ape,rtre
Mhariri:Yusuf Saumu