1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma anusurika tena kutimuliwa uongozini

Jane Nyingi
12 Novemba 2016

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kwa mara nyingine tena amenusurika kura ya kutokuwa na imani nae, kutokana na kile upinzani unachokiita uongozi wake usiowajali raia wa Afrika Kusini kwa kuruhusu ufisadi serikalini.

Südafrika Präsident Jacob Zuma
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kiliwasilisha hoja bungeni kufuatia ufichuzi wa idara ya kupambana na rushwa nchini humo kuwa familia tajiri ya Gupta iliruhusiwa na Zuma kufanya uteuzi wa mawaziri. Wakati ulipoanza  mjadala bungeni kuhusu hoja hiyo ya kutokuwa na imani na rais Zuma, upinzani ulitaka iamuliwe kupitia kura ya siri. Hata hivyo chama cha rais Zuma cha ANC kiliuzima kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge. Upinzani ulipata  kura 126 huku upande wa serikali  ukiungwa mkono na wabunge 214. Matokeo hayo yaliughadhabisha upinzani, na kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani  cha Democratic Alliance  Mmusi Maimane kusema wanasiasa wanaoendelea kumlinda rais Zuma siku moja watajutia walichokifanya “Kura dhidi ya hoja hii ni kura ya kuendeleza ulaji rushwa ,ni kura  ya kukubali wizi, ni kura ya kuruhusu utumizi mbaya wa madaraka. Lazima tuiweke mbele Afrika Kusini.Hebu tuziweke kando tofauti zetu na kuwafikiria watu wa taifa hili kwanza.”

Bunge la Afrika KusiniPicha: picture-alliance/AP Photo/S.van Zuydam

Hii ilikuwa  ni mara ya tatu kufanyika kura ya  kutokuwa na imani na utawala wa rais Zuma katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja. Uchunguzi uliofanywa na idara ya  kupambana na rushwa nchini humo ulipendekeza kundwa jopo la majaji kuchunguza madai ya uhalifu katika serikali ya Zuma. Idara hiyo ilipata ushahidi  kuwa familia ya Gupta iliyo na uhusiano mkubwa na rais Zuma,imekuwa na ushawishi mkubwa katika uteuzi wa nyadhifa mbalimbali serikalini . Inadaiwa hata watu wawili walipewa nyadhifa za uwaziri na familia ya Gupta. Hata hivyo upande wa serikali  umeshikilia kuwa rais Zuma anafanya kila awezalo kukabiliana na rushwa  na pia kuimarisha uchumi wa taifa.Waziri wa  maji na usafi wa mazingira Nomvula Mkonyane  alimtaka kutovunjwa moyo na harakati za upinzani. Kwa rais  Zuma sisi kama African National Congress  tunasema  kamwe dunia haiwezi kutambua  mambo mazuri  unayoyafanya mara millioni, lakini itakukosoa  kutokana na kosa moja unalofanya. Usivunjike moyo.Sisi kama ANC hatuwezi kudai hatuna kasoro,lakini ni kupitia  juhudi zetu tutaendelea kuzingatia maadili na kanuni za chama pamoja na katiba,Hakuna hata mmoja anaweza kudhubutu  kutukosoa  kutona na hilo."

Familia ya GuptaPicha: imago/Gallo Images

 Rais Zuma ,ameendelea kupata ungwaji mkono mkubwa kutoka chama chake cha ANC ambacho kinadhibiti karibu thuluthi mbili  ya idadi ya wabunge 400. Rais huyo amekanusha kuwepo ushawishi wowote wa familia tajiri ya Gupta serikali ambayo inamiliki makampuni mbalimbali katika sekta ya madini na hata vyombo vya habari. Familia  hiyo ya kihindi pia imekanusha kuhusika  katika kosa lolote.

 

Mwandishi Jane Nyingi/Afrika link/APE/AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW