1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma apuuza agizo la kujisalimisha kwa polisi

5 Julai 2021

Rais wa zamani wa Afrika Kusini aliyeagizwa kujisalimisha mwenyewe kwa polisi ili kuanza kifungo cha miezi 15 jela kwa kupuuza amri ya mahakama, amesema hatajisalimisha kufikia muda wa mwisho uliowekwa na korti.

Südafrika l Ehemaliger Präsident Jacob Zuma
Picha: Michele Spatari/AFP

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma aliyeagizwa kujisalimisha mwenyewe kwa polisi ili kuanza kifungo cha miezi 15 jela kwa kupuuza na kutoheshimu amri ya mahakama, amesema hatajisalimisha kufikia muda wa mwisho uliowekwa na korti. 

Zuma amewaambia waandishi wa habari katika makaazi yake ya Nkandla, wilaya ya Kwa-Zulu Natal kuwa hakuna haja ya yeye kwenda jela.

Amesema atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya kumpa adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela pamoja na kuzuia agizo la kukamatwa kwake na polisi.

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 79, amesema kupelekwa jela wakati wa kilele cha janga la ugonjwa wa Covid-19 ni sawa na kuhukumiwa kifo.

Soma zaidi: Zuma asema hana hatia katika tuhuma za rushwa

Zuma amewaambia maelfu ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya makaazi yake ya Nkandla kuwa alinyimwa haki zake za kikatiba na majaji wa mahakama ya katiba nchini humo.

"Siombi kuonewa huruma lakini nataka haki. Umri wangu na hali yangu ya kiafya pamoja na mambo mengine hayakuzingatiwa wakati uamuzi ulipotolewa."

Wafuasi wa Jacob Zuma wakiwa nje ya mahakama ya Pietermaritzburg Picha: Reuters/R. Ward

Timu yake ya mawakili iliiandikia mahakama kudai kuwa hukumu dhidi yake ilikuwa na makosa, kwa nia ya aidha kupunguza kifungo hicho au kuifutilia mbali hukumu yenyewe.

Zuma, aliongoza wafuasi wake kuimba wimbo maarufu wakati wa enzi za kupambana na ubaguzi wa rangi wa "Umshini Wami" ukimaanisha niletee bunduki yangu, wimbo ambao amekuwa akiitumia sana katika mikutano yake ya siasa.

Mamia ya wafuasi wake wamepiga kambi nje ya makaazi yake ya Nkandla kama hatua ya kumuunga mkono.

"Tuko hapa kumlinda Jacob Zuma asikamatwe. Yeyote anayetaka kumkamata lazima atukamate sisi kwanza, ndio maana tuko hapa. Wakija hapa kesho, tukawepo hapa hapa. Hata kama itachukua mwaka mzima, watatukuta hapa. Tutazuia mtu yeyote atakayejaribu kumkamata Msholozi mbele yetu."

Wafuasi hao wameapa kuzua vurugu na kukwamisha oparesheni za serikali iwapo Zuma atafungwa. Kando na kuapa kumlinda Zuma, wafuasi hao wamemtaka Rais Cyril Ramaphosa aachie madaraka.

Mnamo siku ya Jumanne wiki iliyopita, Zuma alitiwa hatiani kwa kosa la kuipuuza mahakama baada ya kukosa kutii amri ya kufika mbele ya tume ya mahakama inayochunguza madai ya rushwa, uhujumu wa taifa na udanganyifu enzi za utawala wake.

Mahakama ilimpa muda wa siku tano kujisalimisha, muda ambao ulikamilika jana Jumapili.