1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma asema sera za fedha hazitabadilika

Isaac Gamba
4 Aprili 2017

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema sera za nchi hiyo kuhusiana na masuala ya fedha hazitabadilika  na kuwa watu nchini humo watapaswa  kuendelea kuwa watulivu baada ya uwezo wake wa kukopesheka kushushwa.

Südafrika Präsident Jacob Zuma
Picha: Reuters/S. Hisham

Hatua hiyo inafuatia tathimini iliyofanywa na taasisi ya Standard and Poor inayoangalia uwezo wa nchi kulipa mikopo yake.

Tathimini ya taasisi hiyo ya Standard and Poor imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya Rais Jacob Zuma kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri ambapo amemuweka kando aliyekuwa waziri wa fedha wa nchi hiyo Pravin Gordhan.

Rais Jacob Zuma hii leo amelitaka baraza lake la mawaziri kuwahakikishia wawekezaji wa kimataifa kuwa mabadiliko aliyofanya ya kumfuta kazi waziri wa fedha Pravin Gordhan  hayatakuwa na athari kwa wawekezaji nchini humo na kusisitiza kuwa kilichobadilika ni uteuzi wa nafasi ya kisiasa pekee bali sera za nchi hiyo kuhusiana na uwekezaji zinabaki kuwa kama zilivyo.

 Amesema mabadiliko hayo yanalengo la kuongeza ufanisi katika serikali ya nchi hiyo kwani ameteua mawaziri vijana wenye uwezo.

Hata hivyo wakati Rais Zuma akitoa kauli hiyo shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini humo Cosatu  limemtaka Rais Zuma ajiuzulu mara moja kufuatia mabadiliko aliyoyafanya katika baraza lake la mawaziri kushusha kiwango cha nchi hiyo kukopesheka.

Katibu Mkuu wa shirikisho hilo la Cosatu Bheki Ntshalintshali amesema ni wakati muafaka  Rais Zuma kujiuzulu kutokana na mabadiliko aliyoyafanya kuonekana kutokuungwa mkono  ambapo katika mabadiliko hayo amemuweka kando aliyekuwa waziri wa fedha ambaye  shirikisho hilo limesema ni waziri aliyekuwa mwenye uwezo na anayeheshimika zaidi. 

 

Cosatu yasema  haina imani na uwezo wa Zuma

Baadhi ya waandamanaji Afrika KusiniPicha: Reuters/S. Sibeko

Amesema shirikisho  la Cosatu halina imani tena na uwezo wa  Rais Zuma  katika kuliongoza taifa hilo na kudai kuwa kiongozi huyo ni mzembe na kuwa kushushwa kwa kiwango cha kukopesheka cha nchi hiyo kutaliathiri taifa hilo kwa kiwango kikubwa.

Msimamo  huo wa shirikisho hilo la vyama vya wafanyakazi nchini humo unakuja mnamo wakati waziri mpya wa fedha wa Afrika Kusini Malusi Gigaba akisema hatua ya kushushwa kwa kiwango cha ukopeshaji  cha nchi hiyo ni pigo  katika sekta ya uchumi nchini humo.

Shirikisho la Cosatu pamoja na chama cha kikomunisti nchini humo na chama cha African National Congress ANC kilikuwa msitari wa mbele katika mapambano ya kuun'goa madarakani utawala wa wazungu wachache ambao ulipelekea kuitishwa kwa uchaguzi mkuu mwaka 1994 na tayari shirikisho hilo linampigia upatu  Makamu wa Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa  aliyeongoza shirikisho hilo wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi kuchukua nafasi ya Zuma pindi atakapolazimika kuondoka madarakani  mwaka 2019.

Sarafu ya randi ya Afrika Kusini imeshuka kwa kiwango cha asilimia tatu kulinganisha na dola ya Marekani kufuatia kushuka kwa kiwango cha kukopesheka cha nchi hiyo.

 Mmusi Maimane ambaye ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Democratic Alliance  amesema kushuka kwa kiwango cha ukopeshaji cha nchi hiyo kutokana na tathimini iliyofanywa na kampuni ya Standard and Poor ni sawa na kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma.

Mwandishi: Isaac Gamba

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW