1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma ataka kumaliza migogoro ANC

8 Januari 2017

Chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC kinahitaji kukomesha malumbano ya ndani na kujikita katika kurejesha imani ya umma, amesema rais Jacob Zuma katika jitihada za kukiunganisha chama hicho kinachozidi kugawika.

Südafrika Präsident Jacob Zuma
Picha: Imago/Gallo Images

Baadhi ya wanachama waandamizi wa ANC wamemtaka Zuma kuachia ngazi, wakitumia hoja ya madoa yaliotiwa kwa chama hicho na kashfa kadhaa za rushwa, kufuatia matokeo mabaya kabisa ya uchaguzi wa manispaa uliofanyika Agosti mwaka uliopita.

Zuma ametuhumiwa pia kwa ufidhuli na kushindwa kutambua kuzidi kupungua kwa umaarufu wa chama cha ANC, baada ya kutoa matamshi juu ya chama hicho kuungwa mkono na "Mungu" na kuongoza hadi "Yesu atakaporudi."

Katika maadhimisho ya mwaka wa 105 wa kuwepo kwa ANC yaliofaynika katika uwanja wa mpira wa Orlando mjini Johannesburg, tukio ambalo kwa kawaida linatumiwa kujipongeza, Zuma alitumia sauti ya upole zaidi.

"Watu wetu wametuambia kwamba tunatumia muda mwingi kupambana wenyewe kwa wenyewe na hatujali mahitaji yao," Zuma mwenye umri wa miaka 74 aliwaambia maelfu ya wafuasi waliokuwa wamevalia fulana za ANC zenye rangi ya njano na kijani.

"Tunapaswa kuwapa watu wetu matumaini, lazima tuungane dhidi ya adui yetu wa pamoja, ambao ni ukosefu wa ajira, umaskini na ukosefu wa usawa, na siyo dhidi ya sisi kwa sisi."

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma ni miongoni mwa wanaopigiwa upatu kurithi nafasi ya Rais Jacob Zuma kama kiongozi mkuu wa ANC baada ya Zuma kuachia nafasi hiyo Desemba mwaka huu.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Migawanyiko inayozidi kukita mizizi ndani ya ANC imechochea mjadala juu ya nani atamrithi Zuma wakati utakapofanyika mkutano mkuu wa chama mwezi Desemba na ambaye pia yumkini akachukuwa hatamu za uongozi wa nchi katika uchaguzi mkuu mwaka 2019, kutokana na udhibiti wa chama hicho.

Wanawake wamuunga mkono Dlamin-Zuma

Tawi lenye ushawishi la wanawake wa ANC siku ya Jumamosi lilisema litamuunga  mkono mke wa zamani wa Zuma na mwenyekiti wa sasa wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma kama mgombea wa kiongozi mkuu wa ANC.

Makamu wa rais Cyril Ramaphosa, mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi aliyegeuka tajiri wa biashara, anatazamwa kama mpinzani wake wa karibu, baada ya vyama vyenye nguvu vya wafanyakazi kutangaza kumuunga mkono mwaka uliopita. Si Dlamini-Zuma mwenye umri wa miaka 67 au Ramaphosa mwenye umri wa miaka 64 alitangaza nia yake ya kugombea.

Julius Malema, mpambe wa zamani wa Zuma na sasa kiongozi mwenye matata wa chama cha msimamo mkali cha Wapiganiaji wa Uhuru wa Kiuchumi EFF, amesema kwamba Zuma anapanga njama ya muhula wa tatu kama rais wa ANC lakini katibu mkuu wa chama hicho Gwede Mantashe alikanusha madai hayo siku ya Jumapili.

Zuma alisema wakati wa hotuba yake kwamba uongozi mpya wa ANC utachaguliwa mwezi Desemba, akiashiria kwamba ataachia ngazi wakati huo. Katiba ya Afrika Kusini inamtaka Zuma kuachia madaraka ya urais wa nchi baada ya kumalizika kwa mihula yake miwili ya miaka mitano kila mmoja mwishoni mwa mwaka 2019.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe

Mhariri: John Juma

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW