1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma kuchunguzwa zaidi

2 Novemba 2016

Ripoti inapendekeza kuundwa kwa tume ya uchunguzi chini ya siku 30 kufanya uchunguzi zaidi

Südafrika Tausende protestieren vor Präsidentenpalast gegen Zuma
Picha: Reuters/M. Hutchings

 Ripoti ya uchunguzi kuhusu ufisadi na ushawishi wa familia tajiri ya Gupta katika serikali ya rais Jacob Zuma imetolewa muda mchache uliopita, baada ya mapema leo, rais Zuma kuondoa kesi ambapo alikuwa akipinga kutolewa kwa ripoti hiyo.

Ripoti hiyo ambayo imemtuhumu Zuma na wakuu wengine serikalini kuhusika kwenye ufisadi kando na kuruhusu ushawishi usiofaa wa familia ya tajiri ya Gupta serikalini, imemtaka rais Zuma kuunda tume ya uchunguzi ndani ya muda wa siku thelathini, na kwamba tume hiyo iongozwe na jaji na ipewe mamlaka ya kukusanya ushahidi ili kufanya uchunguzi zaidi. Kisha imwasilishie rais ripoti hiyo baada ya muda wa siku 180

Aliyekuwa mkuu wa kupambana na ufisadi nchini humo Thuli Madonsela amesema uchunguzi wao umethibitisha kuwa masuala yanayopaswa kuchunguzwa yana upeo mkubwa na yanahitaji uwezeshwaji zaidi ili kufanikishwa, uwezo ambao afisi ya mkuu wa kupambana na rushwa hauna.

Rais Jacob ZumaPicha: Imago/Gallo Images

Mapema leo, jaji Dunstan Mlambo aliamuru kuwa mkuu wa kupambana na rushwa aitoe ripoti hiyo Leo. Hiyo ni baada ya wakili anayemwakilisha rais Zuma kuiambia mahakama kuwa Zuma ameamua kuondoa kesi ambapo alikuwa akipinga kuchapishwa kwa ripoti hiyo iliyopaswa kutolewa Oktoba 14.

Maelfu ya raia wameandamana katika Barabara za mji wa Pretoria kutaka Zuma ambaye amekumbwa na sakata mbalimbali za ufisadi ajiuzulu. Ripoti kutoka kwa mkuu wa kupambana na rushwa nchini humo ilimlaumu Zuma kuiruhusu familia tajiri ya Gupta yenye asili ya kihindi kuwa na ushawishi usiofaa wa kisasa katika serikali yake, ikiwemo kuwaruhusu kuchagua mawaziri. Fana Mokoena ni msemaji wa wanaharakati wa kiuchumi nchini humo. "Amepoteza muda wa mahakama. Aliambiwa itafikia hapa ambapo ataondoa kesi hiyo na amefanya hivyo. Yuko matatani sasa kwa sababu zake. Chama cha ANC kinaongea kwa sauti kuu dhidi yake na jamii, ninafikri amegundua tumefikia mwisho wa safari naye”

Chama kinachotawala cha ANC kupitia msemaji wake Zizi Kodwa kimekubali ripoti kutolewa kikisema ni vyema kulinda demokrasia ya nchi. Chama hicho kimesema kitatoa taarifa yake kesho kuhusu ripoti hiyo baada ya kuisoma kikamilifu. Kwa upande wake, Rais Zuma amesema anasubiri kuichambua ripoti hiyo ndipo aamue ikiwa ataipinga mahakamani au la.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri:Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW